Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alisema jana k
uwa wananchi wanapaswa kuthibitisha matumizi ya ardhi husika
kabla kununua ili kuzuia hasara.
Alisema kuna baadhi ya maeneo yanaonekana ni
mapori ila ni sehemu za wazi au kwa ajili ya huduma hivyo uthibitisho kwa
Serikali za Mitaa na Halmashauri ni nguzo ya kuzuia utapeli na kadhia ya
kubomolewa.
“Watu wengi wanakurupuka tu kupata viwanja na
kujenga. Wengine wanaanza kujenga halafu ndiyo wanaanza kutafuta hati, baadaye
wanakuta eneo lile ni la wazi au la huduma za shule na kutakiwa kubomoa,”
alisema Lukuvi.
“Hakikisha unapata kibali cha kujenga kwa sababu
ukipata kibali unampa kazi mtoa kibali kufuatilia undani wa eneo lako na iwapo
akikuruhusu ujenge halafu mambo yabadilike, watalazimika wakulipe fidia.”
Lukuvi alisema ili kurahisisha mchakato wa upimaji
ardhi, wizara inazidi kusajili kampuni nyingi binafsi za kupima ardhi kwa kuwa
Serikali haina wataalamu wengi wa kupima.
Mbali na kuongeza wapimaji, alisema ataanza
kuzidhibiti bei kubwa za uuzaji wa viwanja zinazotumika sasa na halmashauri
nchini na kusababisha wananchi wengi kukosa viwanja.
Alisema halmashauri zimegeuza upimaji na uuzaji wa
viwanja kama chanzo kikubwa cha mapato huku zikiwanyonya wamiliki wa mashamba
ambayo huchukuliwa kwa kuwapa fidia kidogo.
“Nataka baada ya kupima eneo, wanavyoleta michoro
ya eneo nataka walete na mapendekezo ya bei zao tuzione na kutoa bei elekezi.
“Wananchi wengi wenyeji wameshindwa kununua viwanja kwa sababu ya bei kubwa.
Wao hulipwa fedha kidogo za fidia na kuuziwa kwa gharama za mara 500 au 1,000,
safari hii hatutakubali,” alisema Lukuvi.
Alisema Serikali imeagiza vifaa vingi vya kupimia
ardhi vitakavyowekwa kwenye ofisi tisa za kanda na halmshauri zote zisizokuwa
na vifaa zitakuwa zinaenda kuchukua pale kwa ajili ya kutoa huduma kwa
wananchi.
Katika mipango hiyo mipya, Lukuvi alisema shughuli
za uthamini ardhi na majengo, utoaji wa vibali vya mikopo kupitia ardhi,
usajili na utoaji wa hati zinafanyika ofisi za kanda na kwamba hakuna haja ya
mwananchi kwenda wizarani.
“Kamishna Mkuu wa Ardhi sasa hatatia sahihi mambo
yote yafanyike huko. Nataka muda wa chini kupima hadi kuchukua hati uwe mwezi
mmoja na kipimo cha juu miezi mitatu. Mwananchi yoyote atakayepata hati baada
ya miezi mitatu anijulishe niwashughulikie maofisa wa halmashauri hiyo,”
alisema Lukuvi.
Pia mkurugenzi amesema Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya makazi ya
Space and Development, Renny Chiwa alisema uelewa mdogo katika matumizi ya
ardhi na mipango miji umewafanya Watanzania wengi kujenga kiholela katika
maeneo mbalimbali yakiwamo ya wazi na mabondeni.
“Kwa sasa mtu akiona ardhi tu anataka kujisitiri
bila kuulizia na kufuata taratibu. Serikali na wadau wanatakiwa kutoa elimu ya
kutosha juu ya umiliki wa ardhi na matumizi yake,” alisema.
Chiwa aliwataka wataalamu wa wizara ya ardhi
washirikiane na taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa jamii kama Shirika la Umeme
(Tanesco) na Kampuni ya huduma ya Majisafi (Dawasco) katika kudhibiti
uendelezaji wa maeneo hatarishi na wazi.
Alisema Tanesco na Dawasco wamechangia kwa kiasi
kikubwa kuvutia watu kujenga katika maeneo yasiyotakiwa kwa kuwa waliunganisha
huduma kwa wakazi hao wakati wakijua bayana hapafai.
“Yale maeneo ya mabondeni yote yalikuwa na umeme
na maji ya Dawasco. Wao wanawaza kuongeza wateja na fedha tu lakini kwa nchi
kama Kenya taasisi hizo zinashirikiana na wataalamu wa ardhi kuzuia uendelezaji
huo holela,” alisema.
Njia nyingine ya kukomesha ujenzi holela, Chiwa
alitaja kuwa ni Serikali kuyabaini maeneo yote ya wazi, kuyawekea alama na
kuyaendeleza ili yasivutie watu kuyavamia.
Alisema Serikali inaweza kutafuta wawekezaji wa
sekta binafsi ambao wataendeleza kwa kutoa huduma za burudani katika maeneo
hayo ya wazi kuliko kuyaacha bila kuyaendeleza.
Ili kumaliza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa, Chiwa
alishauri kuchochea ukuaji wa sekta binafsi katika uendelezaji wa ardhi na
makazi kwa kuwa Serikali ina watumishi wachache ambao hawawezi kumudu mahitaji
ya sasa ya upimaji na uendelezaji ardhi.
Chiwa alipendekeza ramani za mipango miji
zipelekwe ngazi za kata badala ya kukaa wizarani na watumishi wa kada za chini
za ardhi wenye elimu ya vyeti na stashahada wapelekwe kila kata kutoa huduma
hizo kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali za mitaa.
“Hii itafanya watu wengi wapime ardhi zao kwa
hiari kwa kuwa hakuna urasimu na hatimaye wataacha kuvamia ardhi na tabia ya
kujenga kiholela bila kufuata mipango miji,” alisema Chiwa.
Ofisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilala, Alfred
Mbyopyo alisema wananchi wanaweza kuepuka kujenga kiholela kwa kununua viwanja
vilivyopimwa au kurasimisha maeneo yao waliyoyanunua kienyeji.
Alisema kwa wale walionunua viwanja vya
halmashauri za wilaya vikiwa vimepimwa na kupatiwa hati wanatakiwa kuandaa
michoro yao kupitia kwa msanifu majengo yoyote na kuipeleka halmashauri kupata
vibali vya kujenga ili kuepusha matatizo.
Mbyopyo alisema kwa wale wanaonunua mashamba au
maeneo kienyeji wanaweza kurasimisha na kupata hati za umiliki sawa na
walionunua viwanja vikiwa vimepimwa wakianzia na ngazi za Serikali za Mitaa.
“Ukishauziwa eneo lako kama ni miguu 20 kwa 20
kama ambavyo wengi hupima unatakiwa uwatafute maofisa ardhi wa halmashauri au
wataalamu binafsi kupima. Ningeshauri wafanye upimaji kwa makundi ili kuokoa
gharama,” alisema.
Kwa wapimaji binafsi alisema, watapata vibali vya
kupima eneo husika kutoka kwa halmashauri ya Manispaa kuruhusu upimaji wa
maeneo husika.
Baada ya kupimiwa na kupata vipimo vya ardhi zao
na kubainishiwa havina matatizo yoyote, wanapaswa waende halmashauri husika kwa
ajili ya kuhakikisha michoro ya eneo na matumizi yake.
Alisema wapimaji hao watachukua nyaraka hizo na
kwenda nazo Wizara ya Ardhi na kupatiwa namba ya kiwanja kupitia idara ya
upimaji.
Baada ya kupatiwa namba mwombaji au mtaalamu wake
watarudi halmshauri kwa ajili ya kibali cha umiliki baada ya ofisa ardhi na
mipangomiji kujiridhisha na mpango wa hati utaandaliwa tayari kupelekwa kwa
Kamishna wa Ardhi wa Kanda kwa ajili ya usajili na hati ambayo hutolewa na
msajili wa ardhi.
Mbyopyo alisema suala la hati halihusishi kundi
kwa waliopima kwa pamoja, bali ni la mtu binafsi kwa kuwa kuna gharama zake,
hivyo ni bora wataalamu waliohusika kupima wakatumika kufanikisha upatikanaji
wa hati hizo.
Kama ilivyo kwa wenye viwanja vilivyopimwa,
Mbyopyo alisema wamiliki wa maeneo ya kienyeji yaliyopatiwa hati na Serikali
watafuata taratibu za kupeleka michoro na kuruhusisha kujenga.
Source mwananchi
Post a Comment