0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara
nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua
mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa
malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna
makontena 2,431 yameto
lewa bila kulipiwa
ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya
ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi
Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila
kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs)
ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu
ambao wamesimamishwa kazi kutokana na
makosa hayo.
“Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na
kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi.
Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato
namna hii,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa
Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini
majina ya watumishi wote waliohusika na
ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni.
Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha
kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa
utozaji malipo kutoka kwenye billing system na
badala yake kuweka mfumo wa malipo wa
kielektroniki (e-payment).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3,
2015), wakati akikagua idara mbalimbali za
mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo
unavyofanyika kwa kutumia scanners.
Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo,
Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema
kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye
kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya
kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben
Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha
scanner, inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa
itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa
kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo
ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa
amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za
Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa
yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya
wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo
ambako alibaini madudu kwenye malipo ya
mishahara na makato ya michango ya
wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi
Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika
kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi
lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na
Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze
miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo.
“Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha
miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini
nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.
“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh.
bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi
ya shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha
hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui
mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi
wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.
Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo
TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema
wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye
mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato
kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai –
Novemba 2014.
Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi
Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri
wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata
mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi
waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya
usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu
wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia
usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia
mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari
jijini Dar es Salaam,” alisema.


Post a Comment

 
Top