Majira
ya saa 7.15 usiku wa kuamkia leo, kundi la watu waliovalia unifomu za kiaskari,
wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa soksi, na kushikilia silaha za jadi kama
mapanga, mikuki, ma
rungu na mapande ya nondo, walivamia kituo cha redio binafsi
na kuteketeza kwa moto studio yake.
Zaidi ya watu 16 waliruka ukuta wa geti na kuingia
ndani ya uwanja wa jengo zilipo ofisi za Hits FM Redio, eneo la Mnara wa Mbao,
Migombani, mjini Zanzibar na kuharakia mpaka sehemu ya nyuma ya jengo kwenye
studio kuu na chumba cha kutengenezea vipindi.
Ndani ya studio, wakati huo vipindi vikiwa
vinaendelea, walimkuta Ali Abdalla akitangaza kipindi cha burudani, na kumtaka
aondoke kutangaza.
“Hapo nilivowaona tu nikajua kuna jambo kubwa
linatokea, sikubishana nao, kwa kuhofia wangeniumiza, niliacha kutangaza na
kuondoka kwenye kiti cha kutangazia,” anasema Ali, mtangazaji kijana
aliyejiunga na Hits FM Redio miezi minne iliyopita.
Ali anasema aliwekwa chini ya ulinzi, akapigwa
mapanga mara kadhaa kwa kutumia upande wa ubapa; akaamriwa kulala chini,
akafungwa mikono kwa nyuma, askari mmoja akamchomeka matambara kinywani.
Akaongozwa nje ya studio huku akiwa amefungwa
kitambaa usoni asione kinachotendeka. Akawa anasikia kelele za wavamizi
wakielekezana cha kufanya.
“Nasikia vishindo huku na kule, nikaanza kusikia
vitu vinavunjwa hivi. Vishindo vikubwa vinaendelea, nikawa nasikia sauti za
watu kama wanakimbia. Baada ya muda nikasikia kimya kizito, nikahisi labda
wameondoka. Nikaendelea kidogo kutulia, nilipojiridhisha kuwa wameshaondoka,
nikajiinua mpaka kufanikiwa kujizongoa. Nikajizoa na kutoka nje ya jengo.”
Wavamizi walichoma moto chumba cha studio na cha
kutengenezea vipindi, baada ya kuvimwagia petroli. Studio iliharibika kabisa,
hakuna kilichonusurika na moto, lakini chumba cha kutengenezea vipindi
hakikushika moto kutokana na kikwazo cha baridi kali iliyokuwa ndani.
Wavamizi waliruka ukuta baada ya kushindwa kufungua
geti. Hakuna mlinzi aliyeibuka walipokuwa wanatoa amri ya kufunguliwa mlango.
Walinzi walikuwepo wawili kutoka kampuni ya Island Security Group, lakini
walijificha waliposikia kundi la watu wanavamia. Walijibanza pembeni mwa eneo
la uwanja wa jengo. Walipoona wavamizi wamepita na kufukuzia nyuma ya jengo
kwenye studio, wakaruka ukuta pembeni na kutoka nje. Walikwenda nyumba ya
jirani kuomba msaada wa askari wa JKU wanaolinda nyumba ya serikali anayoishi Spika
wa Baraza la Wawakilishi. Hawakusaidiwa.
Wakatoka nje barabarani na kwenda kwenye geti la
nyumba ya Rais mstaafu wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambako walinzi
ni askari polisi wa FFU. Wakajieleza na kupata msaada wa kupigiwa simu kituo
cha polisi ambako askari kadhaa walikuja kutoa msaada wakati wavamizi
walishakimbia.
“Sijui hasa kwa nini wametuvamia na kuchoma kituo
chetu. Hatuan chuki na mtu yeyote zaidi ya kufanya kazi zetu kwa uadilifu.
Hatuandami mtu yeyote wala kikundi chochote, tunajiona tunaofanya kazi
wanayoitaka wasikilizaji wetu. Ni bahati mbaya tumehujumiwa namna hii,” ndivyo
alivyosema mtangazaji Abdalla alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Mkuu wa Utangazaji wa Hits FM, Juma Ayoub amesema,
“hatuna bifu na mtu yeyote, tulichotendewa ni uonevu tu na ni jambo la
kusikitisha sana. Itachukua muda mpaka turudi hewani.”
Moza Salum, Mhariri wa Hits FM, amesema
“inasikitisha unapoona migogoro ya wanasiasa inasababisha vyombo vya habari
kuhujumiwa. Wamehujumu wasiohusika na mambo yao. Hii ni hatari kwa kweli.”
Waandishi na wafanyakazi wa kituo hicho wameeleza
kusikitishwa na kilichotokea. Mmoja alisema, “Waliokuja walijiandaa kwa sababu
asiyejua tulivyo hapa kazini hawezi kujua zilipo studio zetu. Labda wametumwa
kuhujumu chombo cha habari hiki.”
Mmiliki wa kituo hicho, Mohamed bin Jabir amesema
wafanyakazi wapatao 22 wakiwemo waandishi na watangazaji na wahandisi
wataathirika kwa kukosa cha kufanya mpaka matangazo yatakaporudi.
Hakujua kwa uhakika itachukua muda mrefu kiasi gani.
Anasikitika uharibifu huo umefanywa siku chache baada ya kufunga vifaa vipya
vya studio katika mpango wa kuongeza ufanisi wa shughuli za utangazaji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP
Mkadam Khamis Mkadam alifika kukagua uharibifu uliofanyika, akifuatana na kundi
la wasaidizi wake. Maofisa wa serikali kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Tume
ya Utangazaji Zanzibar – Zanzibar Broadcasting Commission (ZBC) – walifika
kujionea uharibifu.
Oktoba 27 mwaka huu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kupitia Tume hiyo, ilikifungia kituo cha radio cha Swahiba (Swahiba FM Radio)
kwa madai ya kutangaza matangazo yanayokwenda kinyume cha sheria.
Kituo hicho kilirusha baada ya kurekodi taarifa
aliyoitoa saa kadhaa kabla, Maalim Seif Shariff Hamad kuhusu matokeo ya uchaguzi
akisema alikuwa anaelekea kushinda. Alitangaza hivyo mbele ya waandishi wa
habari, wakiwemo wa vituo vya redio na televisheni waliorusha moja kwa moja
matangazo wakati wa mkutano wa waandishi.
Kituo cha Swahiba FM kinaendeshwa na kampuni
inayomilikiwa na Chama cha Wananchi (CUF). Hata CCM wanaendesha kituo kiitwacho
Bahari FM ambacho kinaendelea na matangazo yake, huku kikisikika kutoa taarifa
za uchochezi. Siku chache baada ya Swahiba FM kufungiwa, watu waliokataa
kujitambulisha ni nani na wanatoka wapi, walifika usiku na kuhoji walinzi na
wafanyakazi waliokuwepo. Waliondoka bila ya kuleta madhara.
Juni 29, askari waliofunika nyuso zao wakiwa na gari
ya moja ya vikosi vya ulinzi vya SMZ walivamia kituo cha redio cha Coconut FM
kinachomilikiwa na kampuni ya Clouds Entertainment ya
jijini Dar es Salaam na kutishia usalama wa wafanyakazi waliowakuta nje ya
jingo eneo la Mnara wa Mbao, Migombani.
Uvamizi huo unaofahamika hapa kufanywa mchana na
askari wa moja ya vikosi vya SMZ, unatajwa kuwa ulifanywa kwa lengo la
kumshambulia mwandishi Ali Mohammed ambaye siku chache kabla, alirusha kipindi
maalum cha kujadili mwenendo wa vitisho uliokuwepo wakati Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) ikiendelea na kazi ya kuandikisha wapigakura.
Mwandishi huyo aliondoshwa kazini kwa kile wengi
walichokieleza kuwa “ni matokeo ya vitisho vya uongozi wa serikali dhidi ya
mmiliki wa kituo.” Inasemekana alipewa sharti kumtimua au akubali kituo
kifungwe.
Askari wa vikosi vya SMZ waliopewa jina jipya la
Mazombi, baada ya Janjaweed lililozoeleka
muda mrefu, wanalaumiwa kwa kuendesha vitendo vya mashambulizi dhidi ya raia
hasa kwenye maeneo wanayohisi yanakaliwa zaidi na wafuasi wa upinzani.
Hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo
ambayo Kamanda wa Polisi Mkadam aliahidi uchunguzi unafanywa wa kujua
waliohusika. Hata hivyo, polisi wamekuwa wakishuhudiwa kuandamana na askari hao
wa vikosi vya SMZ kwa mtindo wa kuwapa hifadhi wakati wanapofanya mashambulizi
mitaani.
Post a Comment