0


Marine Services Company Ltd (MSCL), inadaiwa kutumia kinyume sh.milioni 300 kati ya milioni 600 ilizokuwa imepewa kutengeneza meli ya Mv.Victoria.
 
Hali hiyo iligunduliwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza Magesa Mulongo baada ya kutembelea ofisi za kampuni hiyo zilizopo Bandari ya Mwanza Kaskazini.
 
Uongozi wa MSCL unadaiwa kutumia fedha hizo kulipa mishahara badala ya kutengeneza meli hiyo iliyojengwa mwaka 1964, ambayo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa imeegeshwa katika Bandari ya Mwanza Kusini, kutokana na kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kangavuke (Generator) ya kufua nishati ya umeme melini.
 
Hali hiyo imewaathiri vibaya abiria na wasafirishaji wa mizigo kati ya Mwanza na Bukoba.

Desemba mwaka jana Mv Victoria ilipandishwa kwenye chelezo ili ifanyiwe matengenezo,kazi iliyopaswa kuanza Julai mwaka huu, lakini haikufanyika kutokana na fedha kukosekana; hivyo ikashushwa kutoka kwenye chelezo.

Imedaiwa kuwa matengenezo ya meli hiyo inayotegemewa na wakazi wa Mikoa ya Mwanza na Kagera,yamekwama kutokana na kiasi cha fedha kutumika kulipa mishahara ya wafanyakazi na kiasi kingine kununua vipuri kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa meli nyingine (Mv.Serengeti) kinyume na maelekezo ya serikali.

Mkuu wa mkoa autuhumu uongozi 
RC Mulongo alisema kitendo cha uongozi kujichukulia uamuzi wa kumega kiasi cha fedha hizo bila utaratibu,kimesababisha wananchi wanaosafiri na kusafirisha mizigo yao kati ya Mwanza na Bukoba kwa kutumia meli hiyo, kukosa huduma hiyo sababu ya watu wachache kutofuata taratibu za matumizi ya fedha za umma.

Alisema kama fedha hazikutolewa zote,ilipaswa ifanyiwe matengenezo ya awali wakati mambo mengine ya mishahara yao yakiendelea kushughulikiwa.

"Lakini ninyi mmejimegea chenu kwa madai meli hazifanyi kazi,menejimenti ya kampuni hii imekosa mipango na mikakati na vipaumbele vya kusaidia kubuni na kufufua meli hiyo. Hata kama fedha zitatolewa ni kazi bure," alisema Mulongo.

Kampuni yanena
Mhasibu Mkuu wa MSCL, Beatus Rugarabamu na Kaimu Mrakibu wa Meli, Exavery Kapinga, walisema sababu ya kuchukua kiasi cha fedha hizo na kulipana mishahara ni kuyumba kwa uendeshaji wa biashara kunakotokana na kusimama kwa meli karibu zote za kampuni hiyo, isipokuwa mbili tu, kwa sababu ya uchakavu.
 
Kapinga alisema kampuni hiyo ya huduma za meli za usafirishaji abiria na mizigo iliyoanzishwa mwaka 2009,ina jumla ya meli 14, kati ya hizo tisa zikiwa kwenye Ziwa Victoria, tatu Ziwa Tanganyika na mbili ziko Ziwa Nyasa.
 
Kapinga alisema kati ya meli zote hizo, ni mbili tu zinazofanya kazi tena kwa kusuasua ambazo ni Mv Serengeti ya Ziwa Victoria na nyingine iliyopo Ziwa Nyasa.
 
Alisema ili meli hizo ziweze kutengemaa na kufanya kazi zinahitajika sh. bilioni 8.93 kwa ajili ya matengenezo, ndipo kampuni itapata uhai na kuendelea kutoa huduma kwa faida.

Post a Comment

 
Top