Taarifa iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano Tamisemi,
Rebecca Kwandu, ilieleza kuwa Waziri Simbachawene amemuagiza mkurugenzi wa
Manispaa hiyo kuwasimamisha kazi kaimu ofisa biashara, Elias Kamara na msaidizi
wake, Donatila Vedastus ili kupisha kufanyika uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Simbachawene alichukua uamuzi huo jana baada ya kupokea malalamiko
kutoka kwa wafanyabiashara wa mjini Dodoma na kuyaafanyika kazi na kubaini
tuhuma dhidi ya maofisa hao zina ukweli.
Kwa mujibu wa Kwandu, utekelezaji wa agizo hilo ulianza jana na
kumuagiza mkurugenzi wa manispaa jiyo kukaimisha nafasi zao kuanzia siku hiyo.
“Uchunguzi ambao umefanyika katika manispaa ya Dodoma imegundulika
kuwa kulikuwa na maombi ya leseni 750, ambayo yalikuwa hayajashughulikiwa bila
sababu za msingi na hali hiyo ilipelekea kuikosesha manispaa hiyo kiasi cha Sh
750 milioni,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Simbachawene aliagiza mamlaka za Serikali nchini kuhakikisha
zinatoa leseni za biashara bila ya urasimu na muombaji kupewa leseni ndani ya
siku mbili au tatu tangu alipoomba.
Awali waziri huyo alikutana na waandishi wa habari ofisini kwake
mjini Dodoma, na kueleza mipango ya Serikali katika kufanikisha elimu bure.
Alisema tayari kiasi cha Sh131.4 bilioni zilizotengwa na Rais John
Magufuli kwa ajili ya shule, zimekwishaanza kupelekwa kwa wahusika.
Simbachawene alisema fedha hizo zitakuwa chini ya uangalizi wa
wakuu wa mikoa, wilaya na kamati zao za ulinzi na kuonya kuwa atakayehujumu,
Serikali itamshughulikia ili awe mfano kwa wengine.
Hata hivyo kauli ya waziri huyo jana, bado haikuweza kuondoa
maumivu kwa wazabuni kwani licha ya kutaja kuwa hakutakuwa na madeni ya
kulimbikiza kuanzia Januari mwakani, lakini alisema Serikali haina fedha za
kulipa kwa sasa jambo linalofanya wenye madeni kuongezeka.
Wazabuni wamekuwa wakilalamika ikiwamo kutishia kusimamisha kutoa
huduma kwa taasisi na shule za Serikali kutokana na kile walichokiita kukaribia
kufilisiwa mali zao na taasisi za fedha walikoshindwa kurejesha mikopo.
Post a Comment