Kiasi hicho cha
fedha kimetokana na hesabu inayokadiriwa kuwa matumizi ya waziri iwapo Rais Dk
Magufuli angeendelea na ukubwa wa Baraz
a la Mawaziri la mwisho la Rais Jakaya
Kikwete la mawaziri 55, kati ya hao 24 wakiwa manaibu waziri.
Hata hivyo, Dk
Magufuli ameshatangaza kuwa na baraza dogo la mawaziri, ingawa hajaweka bayana
litakuwa na jumla ya mawaziri wangapi.
Kwa mujibu wa
aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck
Ole-Medeye, Waziri hulipwa mshahara wa kati ya Sh3.8milioni mpaka Sh 5milioni
kwa mwezi ambazo ni sawa na mshahara wanaolipwa wabunge.
Kwa mantiki
hiyo, kwa mawaziri 55, Serikali ilitakiwa ilipe Sh209 milioni kwa ajili ya
mishahara ya Novemba, lakini hazikulipwa kwa kuwa bado kiongozi huyo
hajawateua.
Kanuni za
kudumu za utumishi wa umma toleo la mwaka 2009, zinaitaka Serikali kumpatia
nyumba mtumishi anayetakiwa kupatiwa huduma hiyo kwa aidha kumpa nyumba ya
Serikali au kumkodishia nyingine yenye hadhi ili aweze kutimiza wajibu wake
ipasavyo.
Kanuni hizo
zinamtaka Wakala wa Majengo (TBA) kufanikisha zoezi hilo la kutoa huduma za
nyumba au kusimamia ukodishaji wa nyumba husika ya mtumishi.
Mawaziri ni
miongoni mwa watumishi wanaopatiwa nyumba za Serikali ambazo nyingi
zinapatikana katika maeneo ya vigogo ya Masaki, Oysterbay au Mikocheni jijini
Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa
tovuti ya uuzaji na ukodishaji nyumba na viwanja ya Lamudi, nyumba za bei ya
wastani ambayo inaweza kwenda na hadhi ya waziri inakodishwa kwa kiasi
kisichopungua Sh5 milioni kwa mwezi.
Hivyo basi,
kama nyumba za mawaziri hao ambazo hukarabatiwa na kuhudumiwa na TBA, zingekuwa
zimekodishwa kutoka kwa watu binafsi kwa kipindi cha mwezi mzima basi Serikali
ingelipa Sh275 milioni.
Ili kutimiza
majukumu yao vyema wakiwa bungeni mjini Dodoma, mawaziri pia hupatiwa nyumba za
kuishi tofauti na zile za Dar es Salaam ambazo zipo chini ya TBA.
Hata hivyo,
Ole-Medeye alisema Serikali huwalipa mawaziri Sh800, 000 kwa mwezi kwa ajili ya
huduma za nyumba za Dar es Salaam, mawasiliano na ankara nyingine za kumsaidia
kimaisha.
Iwapo kiwango
hicho cha Sh800, 000 kwa mwezi kingetumika kumlipa kila waziri kama sehemu ya
fedha za makazi, bado Serikali ingehitajika kutoa Sh44 milioni kwa ajili ya
gharama za kuhudumia nyumba na mawasiliano.
“Hivi Sh800,
000 utapata wapi nyumba ya kukodi akaishi waziri? Kwa bei ya sasa nyumba za
kiwango hicho ni Dola za Marekani 3,000 (Sh6 milioni) au zaidi.
“Sasa fedha
hiyo umlipe mtumishi wa ndani, gharama za umeme, mawasiliano na maji ndiyo
maana nasema uwaziri ni kazi ya kuhudumia jamii,” alisema Ole-Medeye akieleza
kuwa waziri hupatiwa posho ya Sh80, 000 kwa siku akiwa mikoani kwenye ziara.
Gharama za
posho za mawaziri hao zingetegemea na siku ambazo wangekaa mikoani kwa kipindi
hicho cha siku 31, na hivyo si rahisi kujua kiwango chake.
Gharama za
samani
Miongoni mwa
mambo ambayo Serikali hugharamia kwa mawaziri wake ni samani za ndani ya
nyumba, ambazo pia huongezeka au kupungua kulingana na ukubwa wa baraza.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema ununuzi wa samani za
ndani ya nyumba za waziri husimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma
(PPRA) kwa wizara zote na hununuliwa kila baada ya miaka mitano.
Hata hivyo, Dk
Meru alitoa angalizo kuwa matumizi ya waziri husika huchangiwa pia na ukubwa wa
wizara na kiwango cha bajeti.
“Mawaziri
wengine wanaishi kwenye makazi yao na siyo wote wamepewa makazi ya Serikali.
“Lakini
wanapewa huduma ya umeme, maji, posho ya majukumu na gari,” alisema Dk Meru.
Mashangingi
Mawaziri pia
hupatiwa magari kwa ajili ya usafiri na mara nyingi huwa na ama Toyota Land
Cruiser VX V8 au GX V8 ambayo hujulikana kama “mashangingi.”
Ili kufanikisha
shughuli zao, kila waziri hupatiwa lita 1,000 kwa mwezi za mafuta. Kwa bei
elekezi ya sasa ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura),
iliyoanza kutumika Desemba 2, bei ya dizeli jijini Dar es Salaam ni Sh1,823 kwa
lita.
Gari moja la
waziri mmoja iwapo lingetumia lita zote 1,000 Serikali ilitakiwa kulipa Sh1.823
milioni ambazo kwa baraza zima ingekuwa jumla ya Sh100.3 milioni.
Pia, magari
hayo huitaji kufanyiwa matengenezo kwa kila baada ya kilomita zinazoshauriwa na
mtengenezaji.
Dk Meru alisema
kwa kawaida kila gari hufanyiwa matengenezo baada ya kilomita 5,000 kwa kiasi
cha wastani Sh1.8 milioni kila moja.
Kwa maana hiyo,
katika Serikali ya “hapa kazi tu” inayohimiza viongozi wa kutoka maofisini
kwenda kusikiliza shida za wananchi vijijini, hapana shaka kuwa mawaziri hao
wangekuwa ama wameshatimiza kilomita zinazohitaji matengenezo au wanakaribia.
Serikali
kufanikisha matengenezo hayo, ingeweza kulipa kampuni husika ya matengenezo
Sh99 milioni kwa mwezi.
Gharama hizo ni
mbali na fedha za kununua magari hayo ambayo kila moja linakadiriwa kugharimu
Sh250 milioni, hivyo mawaziri 55 wangetafuna Sh13.75 bilioni.
Unafuu wa
gharama katika eneo la ununuzi wa mashangingi hayo utakuwa dhahiri iwapo Rais
Magufuli atatekeleza ahadi yake ya kuteua baraza dogo, mathalan, akiteua
mawaziri 20 atakuwa ameokoa mashangi ya mawaziri 35, sawa na Sh8.75 bilioni.
Ukimya wa Rais
Magufuli kutoteua Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha mwezi kumeibua mtizamo
tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya Siasa na utawala, wengi wakisema
kuna faida nyingi kuliko hasara.
Post a Comment