0

Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar, kimedai kuwa na ushahidi mzito, kuhusu namna Uchaguzi Mkuu ulivyoharibiwa kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM (Zanzibar), Waride Bakar Jabu, alipozungumzia mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar jana, akidai wamekusanya taarifa na ushahidi wa kutosha kuhusu mbinu zilizofanyika kuharibu uchaguzi na kusababisha hasara kwa serikali.

Waride alitahadharisdha kwamba, iwapo Zec itaendelea kusuasua kuanika uhalisia wa uchaguzi ulivyofanyika, CCM itaingilia kati kwa kuweka mambo hadharani ili wananchi wafahamu ukweli wake.

“CCM tuna ushahidi wa kutosha jinsi uchaguzi ulivyovurugwa na wapizani wetu, lakini Mungu hakuwa pamoja na wao,” alisema Msemaji huyo wa CCM Zanzibar.

Aidha, Waride alisema kuwa kimsingi CCM inaunga mkono uamuzi wa Zec wa kufuta matokeo na kutangaza kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu.

Alisema kwamba inasikitisha kuona Zec imeshindwa kutangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi kwa wakati na kuwapa wakati mgumu wananchi ambao wanahitaji kufahamu lini watapata haki ya kuchagua viongozi wao akiwamo Rais wa Zanzibar.

Waride alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutagaziwa tarehe ya kufanyika Uhaguzi Mkuu mapema ili wapate nafasi ya kujitayarisha na kujipanga kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wakifuatilia kwa karibu tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio bila kupata majibu tangu Zec kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Pia aliongeza kuwa CCM inaendelea kujipanga na uchaguzi wa marudio, pamoja na kuwashukuru wanachama wake na wananchi walivyojitokeza katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu kabla ya matokeo ya uchaguzi huo kufutwa na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, Visiwani Zanzibar.

Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu huo kwa madai ya kubaini makosa tisa yalifanyika kwenye uchaguzi huo, ikiwamo idadi ya kura kuongezeka kuliko idadi ya wapigakura waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika vituo mbalimbali vya uchaguzi.

Post a Comment

 
Top