Hotuba ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Bungeni baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
30 DESEMBA 2005
Mheshimiwa Spika:
Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya, na akatukutanisha hapa. Ninamshukuru pia kwa Uchaguzi Mkuu wa amani, utulivu na heshima kubwa kwa nchi yetu.
Nakishukuru sana Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa heshima kubwa kilichonipa kwa kuniteua niwe mgombea wake wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ninawashukuru wananchi kwa kunipa mimi na Chama changu ushindi mkubwa sana. Shukrani zangu kwa Watanzania wenzangu—wana-CCM na wasio wana-CCM—ni ahadi ya kuwatumikia kwa uwezo wangu wote.
Nawashukuru wapinzani kwa ujasiri wao mkubwa wa kujitokeza kushindana na Chama Cha Mapinduzi. Uchaguzi sasa umekwisha. Kauli ya wananchi imedhihirika. Tuungane, tuwe kitu kimoja; tujenge na kuendeleza nchi yetu.
Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kumkubali mteuliwa wa CCM kwa nafasi ya Spika, Mheshimiwa Samuel John Sitta, Mb., na pia kwa kukubali uteuzi wangu wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Mb. Naomba mumpe Waziri Mkuu, pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri nitakaowateua hivi karibuni, ushirikiano mkubwa. Wachangamsheni, lakini watendeeni haki na wapeni ushirikiano.
Mheshimiwa Spika:
Nawapongeza Wabunge wote waliochaguliwa. Ninyi, Waheshimiwa Wabunge, ndio macho na masikio ya wananchi. Mmeaminiwa na kuheshimiwa. Naomba kila siku mnapoingia au kutoka katika Bunge hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine wakizungumza, mnapokuwa macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina, kila mara mkumbuke imani na heshima hiyo kubwa mliyopewa na wananchi.
Nakupongeza sana wewe mwenyewe, Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge, na pili kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili Tukufu. Umepata kazi ya heshima kubwa sana, yenye wajibu mkubwa sana. Unao uwezo na uzoefu wa kuifanya. Hivyo, sina shaka utaimudu vema kazi hiyo, na utaliongoza Bunge hili kwa hekima na busara, ukiwatendea haki Wabunge wote, na upande wa Serikali pia. Ninakutakia kila la kheri, na ninakuhakikishia ushirikiano kamili katika kazi zako.
Mheshimiwa Spika:
Ninampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar. Namhakikishia ushirikiano wangu na wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika:
Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Wameonyesha uaminifu kwa Taifa na uzalendo wa hali ya juu. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika:
Wananchi wengi wameelimika na kufuatilia mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na vyombo vya habari. Nawashukuru na kuwapongeza.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.
Mheshimiwa Spika:
Nazipongeza Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa kazi nzuri sana waliyoifanya katika chaguzi zilizopita. Naomba waendelee kunoa uwezo wao, maana Watanzania—Bara na Zanzibar—wanastahili uchaguzi mzuri. Kadhalika tunao wajibu wa kihistoria wa kuwa mfano bora barani Afrika na hata kwingineko.
Siasa
Mheshimiwa Spika:
Chama Cha Mapinduzi kimerejeshwa madarakani kwa kura halali za wananchi zilizotupa idhini ya kutawala, tena idhini kubwa isiyo na shaka hata kidogo. Hatutaona aibu kuitumia idhini hiyo, kupitia Bunge hili, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005.
Kama mwana-CCM nafurahia sana ushindi wetu. Lakini, nikiwa Rais, napenda niwahakikishie wapinzani kuwa hatuna nia au sera ya kuua vyama vya upinzani. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza, kwa dhati, mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi. Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani kwa wapinzani ni kuwa wasiwe wepesi kutafuta mchawi kila wanaposhindwa uchaguzi. Badala yake nawaomba wajiulize kwa nini Watanzania wamewakataa kiasi hicho. Nina uhakika watapata jibu.
Mheshimiwa Spika:
Ni kweli nchi yetu sasa ni ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania. Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na viongozi wake, ikiwemo wale wa Chama Tawala.
Tusipofanya hivyo—na dalili zimeanza kuonekana—wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali nchi mliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.
Mheshimiwa Spika:
Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa. Katika mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie.
Majukumu ya Msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne
Mheshimiwa Spika:
Tangu tupate Uhuru, kila awamu ya uongozi wa taifa imekuwa na majukumu yake ya msingi. Awamu ya Kwanza iliunda na kujenga taifa. Wakoloni hawakujenga hisia za utaifa, maana mkakati wao wa kututawala ulikuwa kutudhoofisha kwa kutugawa ili tutawalike kwa urahisi. Mwalimu Nyerere hakurithishwa taifa na wakoloni. Alirithishwa mkusanyiko wa makabila mbalimbali, na watu wa dini na rangi mbalimbali. Akatambua kuwa hata uchumi wa Tanzania ungekua kwa kasi kubwa kiasi gani, iwapo hakuna misingi imara na hisia za dhati za utaifa, baada ya muda tutasambaratika na uchumi huo utakuwa hauna maana. Kwa kushirikiana na hayati Mzee Karume wakatujengea Taifa la Tanzania lenye umoja, pamoja na watu wake kuwa wa makabila 120, rangi na dini mbalimbali.
Mwalimu aliongoza vita dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Mtandao mkubwa wa huduma za jamii tunaojivunia leo ulianza na falsafa ya maendeleo ya Baba wa Taifa. Wengi wetu tuliomo humu ndani, wa makamo yangu, tusingesoma na kufika hapa tulipo kama si kuona mbali na sera nzuri za Baba wa Taifa. Tutamshukuru yeye na Mzee Karume daima.
Awamu ya Pili chini ya Mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi, ilifungua milango na kupanua uwanja wa ushiriki wa wananchi kwenye uchumi na siasa. Mzee Mwinyi ni muasisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa Tanzania. Alimaliza uhaba wa bidhaa na baadhi ya huduma muhimu uliodhalilisha wananchi. Alipanua sana mipaka ya uhuru wa raia katika maisha yao ya kiuchumi na kisiasa.
Nakumbuka siku moja Mzee Mwinyi alielezea awamu yake kama wakati ambapo mtu anafungua madirisha ya nyumba ili hewa safi iingie ndani. Lakini, akasema, ukifungua madirisha ujue nzi, mbu na wadudu wengine nao wataingia.
Hapo ndipo Awamu ya Tatu ya Rais aliyenitangulia, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ilipoanzia. Ilibidi kushughulikia mbu, nzi na wadudu hao. Rais Mkapa alifanya kazi kubwa kurejesha nidhamu kwenye ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali. Alipiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Alirejesha mahusiano mazuri na wahisani wetu na washirika wetu kwenye maendeleo. Aliweka mazingira bora ya uwekezaji, na ukuaji wa uchumi. Aliimarisha misingi ya uchumi mkuu. Bei za kuruka, na fedha za soksi zikaisha. Ameweka misingi imara ya kuwezesha wananchi kujiendeleza kupitia miradi kama vile TASAF na MKURABITA chini ya mwavuli wa MKUKUTA.
Alikarabati na kupanua sana miundombinu ya elimu, afya, maji na umeme. Barabara na madaraja yamejengwa. Kutokana na juhudi za Rais Mkapa, Serikali ya Awamu ya Nne inaanza bila mzigo wa madeni usiobebeka kama alivyoanza yeye. Tunaanzia mahali pazuri.
Mheshimiwa Spika:
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 imetamka bayana majukumu mawili ya msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne:.
Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea.
Pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umaskini.
Mheshimiwa Spika:
Kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, na mbinu na mikakati mbalimbali ya kuyatekeleza, Watanzania watarajie mambo kumi yafuatayo katika miaka mitano ijayo:
Kwanza, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;
Pili, Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;
Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;
Nne, Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu; itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ya woga wala kuoneana muhali.
Tano, Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;
Sita, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;
Saba, Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;
Nane, Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;
Tisa, Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa maendeleo endelevu; na
Kumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.
Umoja wa Kitaifa
Mheshimiwa Spika:
Umoja wa kitaifa wa Tanzania una pande mbili. Upande wa kwanza ni Muungano wetu; umoja wa nchi zetu mbili huru zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano. Muungano wetu sasa una zaidi ya miaka 41, ni wa pekee barani Afrika. Pamoja na kuwepo matatizo ya hapa na pale Muungano bado ni imara na ni wa kujivunia. Upande wa pili wa umoja wa kitaifa ni umoja wa raia wenyewe, wanaojihisi wote ni Watanzania kwanza, bila kujali tofauti zao za kabila, dini, rangi, jinsia au eneo atokalo mtu.
Kazi mojawapo ya msingi ya Serikali nitakayoiunda ni kulinda, kudumisha, kuendeleza na kuimarisha Muungano wetu, kwa kufanya yafuatayo:
Kwanza, kwa jumla tutakuwa makini na wepesi katika kushughulikia matatizo ya Muungano. Tutayazungumza kwa uwazi na kuchukua hatua muafaka kwa wakati muafaka;
Pili, nitampunguzia Makamu wa Rais majukumu ya kuondoa umaskini ili apate muda wa kutosha wa kushughulikia masuala ya Muungano;
Tatu, nitaimarisha taratibu zilizoanzishwa na Serikali zilizopita za kujadili, kuainisha na kutatua matatizo ya Muungano; na
Nne, nitaangalia upya mchango wa Serikali ya Muungano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, bila kuathiri haki na mamlaka kamili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya Muungano.
Mheshimiwa Spika:
Kwa upande mwingine, umoja wa Watanzania unahusu umoja miongoni mwa wananchi. Ipo hofu ya kweli miongoni mwa Watanzania kuwa bado wapo miongoni mwetu watu wanaotaka kuturudisha tulikotoka, tuanze tena kuulizana na kubaguana kwa misingi ya kabila zetu, rangi zetu, dini zetu, na maeneo tunayotoka. Nawasihi sana wanaowania uongozi, kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya kitaifa—uwe uongozi wa kiserikali, uongozi wa kisiasa au uongozi wa kidini—wasitumie ubaguzi wa aina yeyote ile. Hawatavumiliwa na hawataachwa waigawe nchi.
Mheshimiwa Spika:
Nasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa kati ya Unguja na Pemba. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 yamedhihirisha mpasuko huo ambao naamini chanzo chake ni cha kihistoria. Lakini historia hiyo ni ya wanadamu, na wanadamu hawalazimiki kuwa wafungwa wa historia yao. Iweje Wapemba hawa ambao ni hodari wa kutumia fursa ya Muungano wetu kwa kuishi na kufanya biashara na kuwekeza katika pembe zote za Jamhuri yetu wawe hao hao wanaojitenga kisiasa kwa kiwango tulichoshuhudia kwenye Uchaguzi Mkuu?
Wakati umefika sasa wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko huo. Nategemea ushirikiano mzuri kutoka kwa wanasiasa wa Tanzania-Zanzibar. Natambua kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya siasa na utawala Zanzibar ni wa Wazanzibari wenyewe. Lakini, Jamhuri yetu ni moja, na yanayotokea Zanzibar yanatugusa sote. Pengine leo ni zaidi kuliko ilivyokuwa katika historia wakati ulipokuwepo msemo kuwa zumari likipigwa Zanzibar wanacheza mpaka bara. Hivyo, basi, nitakuwa tayari kuanzisha, kuwezesha na kusaidia mjadala mpana juu ya mustakabali wa kisiasa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge:
Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia, miongoni mwa mambo mengine, kuimarisha utaifa wetu kwa kufanya mambo kumi yafuatayo:
Kwanza, kutumia mfumo wa elimu kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, ikiwemo kutenga Shule za Sekondari za Kitaifa zitakazochanganya kwa makusudi wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutoka pembe zote za Tanzania;
Pili, kuandaa mitaala ya somo la uraia itakayopanda mbegu za uzalendo na umoja wa kitaifa katika ngazi zote za elimu;
Tatu, kuzipa changamoto shule za mashirika ya dini, isipokuwa seminari, kupokea wanafunzi wa dini zote;
Nne, kuendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu ya kufufua Jeshi la Kujenga Taifa;
Tano, kujenga muafaka baina ya vyama na makundi ya jamii juu ya utambuzi wa, na kuheshimu, tunu za kitaifa kama vile haki, usawa, umoja na mshikamano;
Sita, kutumia michezo, nyimbo na sanaa kuimarisha hisia za utaifa na kujenga uzalendo na kuipenda nchi;
Saba, kueneza na kuruhusu matumizi ya alama za kitaifa kama mambo ya kila raia kujivuna nayo na kuyaheshimu sana;
Nane, kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya dini, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya jamii;
Tisa, kuteua Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais atakayeshughulikia mahusiano kati ya vyama vya siasa, dini na makundi mbalimbali ya jamii; na
Kumi, kuimarisha utaratibu wa mazungumzo ili kutatua mapema migogoro katika jamii.
Amani na Utulivu
Mheshimiwa Spika:
Zipo sababu kwa nini nchi yetu imekuwa, kwa kiwango kikubwa, kisiwa cha amani na utulivu katika bahari iliyotibuka. Mojawapo ya sababu hizo, kama nilivyosema, ni sera ambazo kwa makusudi zilijenga hisia za umoja, na hazikuwabagua wala kuwanyima haki Watanzania kwa sababu za dini, rangi, kabila, jinsia au eneo wanakotoka. Nitawatarajia watakaokuwa kwenye Serikali nitakayoiunda wasiwabague wananchi kwa sababu yoyote ile, na wawe watetezi thabiti wa haki za binadamu. Ningependa pia tuwe na maadili na miiko ya kitaifa kuhusu jambo hili.
Utawala Bora
Mheshimiwa Spika:
Serikali nitakayoiongoza itazingatia na kuendeshwa kwa misingi ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji. Tutaheshimu utawala wa sheria, na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola, yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama na Bunge; tutatimiza ipasavyo wajibu wetu; na tutawezesha mihimili hiyo kufanya kazi zake ipasavyo. Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha utendaji Serikalini na kupambana na maovu katika jamii bila woga wala kuoneana muhali.
Rushwa
Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake. Tutajitahidi kuongeza mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya Serikali hasa katika manunuzi na mikataba. Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa, hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi na Mahakama. Lakini yote hayo ni bure iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo. Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi.
Katika harakati za kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na Serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji. Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta utajiri.
Kadhalika, hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali. Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi yako ya utumishi au uongozi wa umma kujipatia manufaa ya kujitajirisha au kujilimbikizia mali.
Jambo hili ndilo linalokera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote lakini miezi michache tu baada ya kupata cheo anakuwa tajiri mkubwa. Ona majumba ya fahari, ona madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na kadhalika. Wananchi wanayo haki kuhoji, na wanayo haki kupata majibu. Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane. Nataka Tume ya Maadili ya Viongozi isione haya kutuuliza jinsi tulivyozipata mali tunazosema tunazo. Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo kama tatizo lenu ni hilo.
Utendaji Serikalini
Mheshimiwa Spika:
Dhana ya utawala bora ni pana sana; ni zaidi ya vita dhidi ya rushwa. Tutahimiza utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ustadi, kwa haraka na kwa ufanisi. Tunataka watendaji wa Serikali wenye wawe waadilifu, na wanaowajibika; wawe na ari, moyo, na msimamo wa dhati kuhusu utumishi wa umma na huduma bora kwa umma. Tabia ya “Njoo kesho” na nenda rudi tuache. Mwalimu alituasa linalowezekana leo lisingoje kesho. Napenda huo uwe moyo wa utendaji Serikalini.
Natambua tatizo na malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu mishahara na maslahi yao. Tutaliangalia. Tutalishughulikia. Nakusudia mapema iwezekanavyo niteue Tume ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma. Naomba niwatahadharishe kutokana na matumaini ya miujiza. Tutafanya kinachowezekana kadri uwezo wa Serikali unavyojengeka.
Mahakama
Mheshimiwa Spika:
Serikali nitakayoiunda, pamoja na kuheshimu uhuru wa Mahakama, itatimiza ipasavyo wajibu wake na kuimarisha miundombinu ya kutoa haki kwa kuongeza idadi ya watumishi, kuwaendeleza kitaaluma, kukarabati majengo yaliyopo na kujenga mapya, na kupeleka huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika:
Kusimamia vizuri mapato na matumizi ya Serikali nayo ni sehemu ya utawala bora. Isitoshe, utekelezaji mzuri wa jukumu hilo ndio unaipa Serikali uwezo wa kutekeleza mengine yote inayopaswa au inayokusudia kuyatekeleza. Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, iliongeza mapato ya Serikali mara tano sambamba na kuweka mfumo mpya na wa kisasa wa kudhibiti matumizi, na kuongeza uwazi katika bajeti ya Serikali. Hatutalegeza kamba hata kidogo. Hatutavumilia wanaokwepa kulipa kodi stahiki za Serikali au wabadhirifu wa fedha na mali za umma. Sheria ya Fedha, na Sheria ya Manunuzi ya Umma, lazima zifuatwe. Watakaokiuka wachukuliwe hatua za nidhamu. Wasiorejesha masurufu ya safari nao wasivumiliwe.
Kazi za Serikali kwenye Uchumi wa Soko
Mheshimiwa Spika:
Utawala bora ni pamoja na Serikali kufanya vizuri kazi zake nyingine muhimu katika mazingira ya uchumi wa soko. Jukumu la msingi la Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri kwa uchumi kukua na biashara kustawi. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Awamu ya Nne itatekeleza mambo manane yafuatayo:
Kwanza, kuweka sera na mazingira bora ya kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi;
Pili, kuweka sera nzuri zinazowezesha ukuaji wa uchumi wa kisasa;
Tatu, kuweka mfumo mzuri wa usimamizi wa mazingira ili kulinda uhai wa binadamu na viumbe hai;
Nne, kuweka mifumo bora ya kusuluhisha haraka migogoro ya kibiashara;
Tano, kuweka utawala mzuri wa sheria na wa haki;
Sita, kuwa na taasisi za kudhibiti na kusimamia viwango vya huduma na bidhaa;
Saba, kuwa na sera nzuri za kifedha ili kuhamasisha uwekezaji na uzalishaji; na
Nane, kutekeleza kwa dhati sera ya uwezeshaji wa wazawa.
Uchumi Endelevu wa Kisasa Unaokua
Mheshimiwa Spika:
Serikali ninayoiongoza itatoa kipaumbele katika kujenga uchumi endelevu, wa kisasa, unaokua. Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa katika eneo hilo, na kutuachia msingi imara ambao sisi tutajenga juu yake. Hatutabomoa msingi huo bali Serikali itatumia mafanikio hayo kama nyenzo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika:
Sekta binafsi ndiyo mhimili wa uchumi wa nchi yetu hivi sasa. Serikali ya Awamu ya Tatu imeweka mazingira mazuri ya ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa. Aidha, Serikali ya Awamu ya Tatu imejenga mahusiano mazuri na sekta binafsi ambayo sasa imepewa fursa ya kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kazi hiyo nzuri. Tutajitahidi kuwa karibu na sekta binafsi kwa maslahi ya nchi yetu.
Kilimo
Mheshimiwa Spika:
Kilimo ndiyo sekta inayoajiri watu wengi na ndiyo inayotuhakikishia upatikanaji wa chakula, bidhaa za kuuza nje na malighafi za viwanda. Vilevile, uhai na maendeleo ya sehemu kubwa ya wananchi yanategemea kilimo. Hivi sasa, Serikali inatoa ruzuku kwenye mbolea na vilevile unafuu wa kodi kwenye pembejeo za kilimo na mifugo. Mpango huo utaendelezwa na kuimarishwa zaidi.
Aidha, Serikali itahakikisha kuwa Mpango Kabambe wa Umwagiliaji Maji unaongezewa fedha na wataalam. Tutahakikisha kuwa utaalam wa asili wa kilimo cha umwagiliaji unafufuliwa, pamoja na miundombinu yake. Huduma muhimu za ugani na masoko zitapewa kipaumbele na msukumo maalumu.
Mheshimiwa Spika:
Tutachukua hatua za dhati kuboresha ufugaji wetu. Hatuna budi tutoke kwenye uchungaji wa kuhama-hama na kuwa wafugaji wa kisasa. Tutachukua hatua za kuboresha malisho na huduma za madawa, majosho na minada.
Tanzania ina mifugo mingi sana, na tukiboresha ufugaji, itatoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa na maendeleo ya wafugaji. Serikali pia itawawezesha wavuvi wengi iwezekanavyo kupata zana bora na vifaa muhimu vya uvuvi wa kisasa ili waweze kutumia kwa ukamilifu eneo la bahari, maziwa na mito ambalo tumejaliwa kuwa nayo.
Viwanda Vidogo na vya Kati
Mheshimiwa Spika:
Katika maendeleo, uchumi wa taifa siku zote unaongeza mchango na viwanda katika pato la taifa. Nasi hatuna budi tufanye hivyo. Viwanda—vikubwa, vidogo na vya kati—vina uwezo mkubwa wa kukuza uchumi, kutoa nafasi za ajira, lakini vilevile vinasaidia kusindika mazao ya kilimo, kuyaongezea thamani na kuzuia yasiharibike wakati wa mavuno. Serikali ya Awamu Nne itatengeneza mkakati kabambe wa kutekeleza sera ya viwanda nchini. Tutachukua hatua za makusudi za kukuza sekta ya viwanda nchini.
Serikali itaendeleza na kuimarisha utoaji wa mikopo kwa viwanda vidogo na vya kati chini ya mpango wa mikopo, na dhamana kwa mikopo, kwa sekta hiyo ambao unasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Shirika la Viwanda Vidogo nalo litapewa uwezo zaidi wa kumudu kazi za kutoa elimu, ushauri, uwezeshaji na usimamizi.
Sayansi na Teknolojia
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itahimiza matumizi ya sayansi na teknolojia, na kuwekeza katika utafiti. Aidha, Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kwa ajili ya taasisi na asasi mbalimbali zinazoshughulikia utafiti wa kiteknolojia. Mfuko wa Taifa wa Sayansi na Teknolojia utaimarishwa kwa kuongeza mchango wa Serikali na kuwahamasisha wadau wengine kuchangia.
Mheshimiwa Spika:
Teknolojia ya habari na mawasiliano imewezesha elimu, taarifa na habari kuvuka mipaka na hivyo kusaidia kupunguza pengo la habari na elimu lililopo kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tutaongeza kasi ya kuandaa mazingira yatakayotuwezesha kutumia teknolojia hii.
Uchumi Unaoshirikisha Raia Wengi
Mheshimiwa Spika:
Mageuzi ya uchumi yameongeza tofauti ya mapato miongoni mwa wananchi. Tofauti hizo zisiposhughulikiwa zinaweza kuwa chanzo cha migogoro na mitafaruku katika jamii.
Jawabu si kuwanyang’anya walio nacho na kuwagawia wasio nacho. Jawabu sahihi ni kuwasaidia wasio nacho wajikwamue, na wainue hali za maisha yao. Changamoto kubwa ni jinsi gani tunaongeza fursa kwa wasio nacho, na kuchochea utayari wao kutumia fursa hizo.
Mheshimiwa Spika:
Kurekebisha na kutengemaza uchumi ni hatua ya mwanzo tu katika safari ndefu ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Serikali ya Awamu ya Nne itaendelea na hatua inayofuata ya kuongeza ushiriki wa Watanzania walio wengi katika uchumi wa Taifa lao. Wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza juhudi zilikuwa kuwafanya wananchi wamiliki uchumi wa Taifa lao kupitia mashirika ya umma. Leo tunataka kufikia lengo hilo hilo la wananchi kumiliki sehemu kubwa ya uchumi wa Taifa lao, moja kwa moja, au kupitia vyama huru vya ushirika.
Mheshimiwa Spika:
Kwa kifupi Serikali ya Awamu ya Nne itaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya wafanyabiashara na wawekezaji wadogo wadogo, kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
Kwanza, kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa kutoa leseni za biashara;
Pili, kurekebisha mifumo ya udhibiti ili udhibiti usizuie sekta binafsi kukua;
Tatu, kuandaa mazingira mazuri ya kufikisha taarifa muhimu kuhusu masoko, kuhusu ubora wa viwango vinavyotakiwa, na kuhusu masharti mengineyo kwa wafanyabiashara na hasa wafanyabiashara wadogo na wa kati;
Nne, kuitaka mikoa ianzishe vituo vya kufanikisha biashara na uwekezaji mikoani, pamoja na Mabaraza ya Biashara ya Mikoa;
Tano, kuboresha mazingira ya biashara na ujasiriamali, ikiwemo kutoa msaada na upendeleo maalum kwa mikopo midogo midogo na ya kati hasa kwa vijana, wanawake na Watanzania wanaohangaika kujikwamua kimaisha;
Sita, kuboresha miundombinu inayogusa shughuli za wafanyabiashara wadogo na wa kati;
Saba, kuhamasisha, kuhimiza na kutoa motisha kwa shughuli za usindikaji nchini ili kuongeza thamani ya mauzo nje; na
Nane, kuhamasisha, kuhimiza na kutoa motisha kwa mafunzo ya ufundi ili kuongeza tija na ufanisi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itaongeza kasi ya kupambana na umaskini. Tutawezesha Watanzania kwa makundi. Kundi la kwanza ni la Watanzania wasomi, walio ndani au nje ya nchi yetu. Zamani ilikuwa mtu ukitoka Chuo Kikuu, kazi ya Serikali inakungoja. Leo hali si hiyo. Wengi inabidi watafute kazi kwenye sekta binafsi, au wajiajiri wenyewe.
Napenda leo nitoe changamoto na ahadi kwa wasomi wetu hao, wenye fani mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, uhandisi, ubunifu wa majengo, sheria, uhasibu na kadhalika. Katika dunia ya utandawazi na ushindani unaoambatana nao, Watanzania wasomi watabaki nje iwapo hawatakuwa wabunifu zaidi, wakaungana na kuanzisha kampuni kubwa za wazalendo.
Lakini wakikubali kuungana, na kuanzisha kampuni kubwa zinazoendeshwa kwa misingi halisi ya kibiashara, na sio ubabaishaji, Serikali, kupitia vyama vya taaluma zao, itawaunga mkono, itawasaidia na itawawezesha. Serikali ya Awamu ya Nne itakaribisha mawazo kutoka kwa vyama vya kitaaluma juu ya namna bora ya Serikali kufikia lengo hilo. Ninataka wasomi wetu wawe kiini cha wajasiriamali wasomi na wakubwa nchini.
Kundi la pili la Watanzania tutakaowasaidia na kuwawezesha ni la wenye miradi midogo sana, miradi midogo na miradi ya ukubwa wa kati. Mazuri mengi yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu, kama vile sera ya uwezeshaji wananchi, sera ya uwekezaji mdogo na wa kati, na mfuko wa udhamini kwa mikopo ya mitaji midogo na ya kati. Yote haya, na mengine mengi, tutayaendeleza kwa jitihada kubwa.
Kundi la tatu ni la wakulima wadogo, wavuvi wadogo na wafugaji wadogo. Hatuwezi kushinda umaskini bila kuwasaidia watu wa kundi hili ambao ndio wengi zaidi. Nitahitaji kuona ubunifu wa hali ya juu kutoka kwa nitakaowakabidhi kusimamia sekta hizi kufanikisha azma yetu hii.
Mheshimiwa Spika:
Yote haya yatawezekana tu iwapo Watanzania watabadili mtazamo wao kuhusu nafasi yao, na nafasi ya Serikali, katika kukuza uchumi wa Taifa na uchumi binafsi. Waswahili husema, ukibebwa na wewe shikilia. Maisha bora hayaletwi na Serikali peke yake; yanaletwa kwa ubia kati ya Serikali na wananchi. Naomba tuimarishe ubia huo katika Awamu ya Nne ya Uongozi wa Taifa letu.
Ajira na Viwanda
Mheshimiwa Spika:
Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM tulijiwekea lengo la kuongeza nafasi za ajira milioni moja katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Nafasi hizi za ajira zinatarajiwa kupatikana Serikalini na katika sekta binafsi. Upanuzi wa sekta za afya, elimu, kilimo, ujenzi wa nyumba na barabara, usindikaji wa mazao na bidhaa asilia, samaki, na utalii ndilo tumaini kuu la ajira. Aidha, matarajio mengine makubwa ya ajira ni kutoka katika sekta isiyo rasmi, yaani ajira binafsi. Tunasisitiza ahadi yetu ya kuchukua hatua thabiti za kuwasaidia vijana, wanawake na Watanzania kwa jumla kupata mikopo na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri. Lengo letu ni kuwa kila raia awe na chanzo cha uhakika cha kipato, na kuibua maeneo mapya ya kuwapatia ajira wananchi wengi zaidi.
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza pia juhudi za kuhimiza, na kuwezesha, uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kama vile vya nguo na vya kuunganisha bidhaa za matumizi ya nyumbani vyenye uwezo mkubwa wa kutoa nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Tatu ilibuni mradi uitwao Tanzania Mini-Tiger Plan 2020 ambao kwa kutumia maeneo maalum ya uchumi utaongeza mauzo nje ya nchi, na kuongeza haraka nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Nne itautekeleza mradi huo kwa ukamilifu.
Ushirika
Mheshimiwa Spika:
Ushirika ni nguzo muhimu ya kuwawezesha wanyonge kuwa na sauti na hivyo kuweza kupambana na umaskini. Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa na nzuri ya kuunda upya ushirika nchini kwa kuhuisha sera na sheria ili kuweka mazingira yatakayochochea kujengeka kwa vyama huru vya ushirika vinavyomilikiwa na kuendeshwa na wanaushirika wenyewe. Serikali ninayoiongoza itaendeleza juhudi hizo pamoja na kuendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kujiunga na vyama hivyo.
Huduma ya Jamii
Kuendeleza huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na kadhalika itaendelea kuwa kipaumbele cha juu cha Serikali ya Awamu ya Nne.
Elimu
Mheshimiwa Spika:
Kazi kubwa ya kupanua miundombinu ya elimu nchini imefanyika katika miaka kumi iliyopita chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu. Uandikishaji wa wanafunzi, wa kike na wa kiume, katika ngazi zote za elimu umeongezeka sana. Elimu itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne, ambayo itafanya yafuatayo:-
Kwanza, kuendelea kuandikisha watoto wote wa rika lengwa la kuanza shule;
Pili, kuboresha taaluma ili kuongeza viwango vya kufaulu;
Tatu, kuongeza ajira ya walimu wa elimu ya msingi na sekondari;
Nne, kushirikiana na wazazi na wadau wengine wa elimu kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo;
Tano, kuongeza ruzuku inayotolewa hivi sasa kwa ajili gharama za kuendesha shule;
Sita, kuimarisha taasisi za kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa;
Saba, kutoa fursa na motisha kwa sekta binafsi, taasisi za dini na mashirika binafsi yanayowekeza katika elimu;
Nane, kuimarisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iweze kutoa mikopo kwa wahitaji wengi zaidi;
Tisa, kujenga angalau chuo kikuu kingine kipya; na
Kumi, kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanaendelezwa na kuimarishwa kama mkakati wa kupambana na tatizo la ajira.
Kumi na moja, kuboresha maslahi ya walimu katika shule na vyuo hapa nchini.
Maji
Mheshimiwa Spika:
Tatizo la maji ndicho kilio kikubwa cha Watanzania mijini na vijijini. Ndiyo kero nambari wani. Serikali za awamu zote zimefanya jitihada kubwa kukabiliana na tatizo hilo. Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia kulikabili tatizo hili kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
Ni makusudio yangu kuwa tuwe na Mpango Kabambe wa Maji kwa nchi nzima. Mpango ambao utajumuisha mikakati na mbinu mpya za kutekeleza kwa kasi Sera ya Maji na kutatua tatizo la maji. Aidha, tutakamilisha miradi mikubwa ya ukarabati na upanuzi wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, na ule wa kupeleka maji katika miji ya Kahama, Shinyanga na vijiji vitakavyopitiwa na bomba kutoka Ziwa Victoria.
Afya
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Tatu imechukua hatua mbalimbali kuboresha sekta ya afya, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Tutaendeleza hatua hizo. Huduma ya afya kwa kina mama na chanjo mbalimbali kwa watoto zitaendelea kutolewa na kuboreshwa zaidi. Tunataka kila mtoto wa Kitanzania apate chanjo zote zinazostahili.
Aidha, tutaimarisha mtandao wa kusambaza dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, pamoja na kuendelea kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa vya tiba. Ukarabati na ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati utaendelea. Kwa kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba tutakazania pia elimu ya afya. Mapambano dhidi ya malaria na kifua kikuu yatapewa msukumo maalum.
UKIMWI
Mheshimiwa Spika:
Nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la UKIMWI. UKIMWI ni janga la kitaifa na dunia kwa ujumla. Janga hili limekuwa likiathiri utendaji na kupunguza nguvukazi ya Taifa. Tutaendeleza jitihada za kuhamasisha na kutoa elimu ya UKIMWI kwa wananchi wote ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anao uelewa sahihi wa janga hili. Aidha, Serikali itatenga rasilimali zaidi, na kushirikiana na wadau mbalimbali, kuongeza upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha na kupunguza makali kwa watu wengi zaidi walioathirika na UKIMWI.
Makundi Maalum
Mheshimiwa Spika:
Katika jamii yetu yapo makundi maalum ambayo Serikali inao wajibu wa kuwasaidia. Kundi la kwanza ni la watoto yatima. Tunahitaji wadau mbalimbali wakae pamoja na kuandaa mipango endelevu ya kuwalea na kuwasaidia watoto hawa. Watoto yatima wanahitaji elimu, lishe bora, huduma za afya, makazi na upendo sawa na watoto wengine wa Kitanzania. Serikali ya Awamu ya Nne inaahidi kuwa yatima watapata elimu na huduma ya afya kwa kusaidiwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika:
Kundi jingine maalum ni lile la walemavu. Zipo hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa kuwapa fursa walemavu kutumia vipaji vyao ili kujitegemea. Changamoto kubwa kwetu kama Taifa ni kuwa tuache kuwanyanyapaa na tuwaone kuwa ni binadamu wenzetu. Serikali itachukua hatua za kuhuisha sera na sheria ili kutoa upendeleo maalum kwa walemavu katika utoaji wa huduma mbalimbali na vilevile katika kuweka mazingira yatakayowapa fursa ya kutekeleza majukumu yao kwa jamii.
Mheshimiwa Spika:
Lipo pia kundi la wazee wetu. Wazee ni hazina kubwa ya Taifa lolote. Jamii yeyote iliyostaarabika inalo jukumu la kuwaenzi na kuwatunza wazee, tukianza na wanafamilia na wanajamii wa karibu wa mzee anayehusika. Wasikwepe jukumu hilo asilia, na la mila za Kiafrika. Serikali itahakikisha kuwa kunakuwepo utaratibu na mipango itakayowawezesha wazee kupata huduma muhimu kwa wepesi zaidi na kwa gharama nafuu, kwa kuzingatia taratibu, mila na utamaduni wa jamii zetu.
Mheshimiwa Spika:
Serikali itazingatia nafasi ya wanawake katika maendeleo. Tutaongeza, awamu kwa awamu, ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi wa kisiasa, kiutendaji na nafasi nyingine za maamuzi. Kadhalika, tutatekeleza ahadi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Utalii
Mheshimiwa Spika:
Serikali yangu inakusudia kuendeleza sekta ya utalii ili iongeze mchango wake kwenye pato na maendeleo ya taifa letu. Tunapaswa kuboresha huduma kwa watalii kama vile malazi, chakula, usafiri na bidhaa za kumbukumbu za kuwauzia watalii. Tunapaswa kukaribisha wawekezaji wa ndani na nje watakaojenga hoteli zenye hadhi ya kimataifa kuanzia nyota nne hadi tano. Tunahitaji kujenga miundombinu ya kuwafikisha watalii katika maeneo ya kitalii kwa urahisi.
Hifadhi ya Mazingira
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itatoa msukumo maalum kwa hifadhi ya mazingira kwani athari zake pale tulipopuuzia zinaonekana wazi. Mvua haba, raslimali maji inazidi kupungua, na ukame unaongezeka. Serikali itaendelea kuthamini na kulizingatia suala hili, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa wao kuhusu hifadhi ya mazingira. Tutaiongezea Wizara inayohusika na mazingira uwezo na mamlaka ya usimamizi. Tutaendeleza kampeni ya upandaji miti na kuhimiza tabia ya kutokata miti ovyo, au kuchoma misitu ovyo. Ili kupunguza mahitaji ya kuni na mkaa tutaendeleza matumizi ya nishati mbadala.
Miaka arobaini tu iliyopita, Tanzania Bara ilikuwa bado na misitu mingi, chemchem na vijito vingi. Sehemu kubwa ya ardhi yake ilikuwa imefunikwa na majani. Leo hali ni tofauti, na kwenye baadhi ya maeneo hali inatisha.
Mheshimiwa Spika:
Uchomaji misitu na ukataji ovyo wa miti vimesababisha vyanzo vya maji kukauka, mito kupungua maji na baadhi ya viumbe kuathirika na kutoweka. Hatuwezi kuendelea kuwa watazamaji au washangaaji wa vitendo hivi vya hujuma dhidi ya misitu na uhai wa taifa letu. Na wala uhuru wa Mtanzania kuishi popote katika nchi yake haujumuishi pia uhuru wa kuharibu mazingira sehemu fulani na kuhamia sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika:
Yapo maeneo ambayo lazima zichukuliwe hatua maalum za kulinda na kuhifadhi mazingira kwani hali imeanza kuwa mbaya sana. Eneo mojawapo ni Bonde la Mto Ruaha ambalo linahusisha vyanzo vya mito yote mikubwa nchini. Tumeshuhudia hali ya bwawa la Mtera inavyoendelea kuwa mbaya. Aidha, mto Ruaha Mkuu umeanza kukauka katika baadhi ya maeneo. Itabidi uongozi wa Serikali katika ngazi zote uwajibike zaidi kuhakikisha kuwa uharibifu wa mazingira unaosababisha hali hii ya kutisha unakomeshwa.
Eneo jingine ni lile linalozunguka Ziwa Victoria. Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kuwa pamoja na umuhimu wa ziwa hilo, uchafuzi wake unaongezeka. Serikali itahakikisha kuwa uongozi wa mikoa yote inayozunguka ziwa hilo unashirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa na wananchi kuhifadhi ziwa hilo linalotegemewa na idadi kubwa ya wananchi wetu.
Uchumi Unaopaa
Mheshimiwa Spika:
Baada ya mafanikio ya Awamu ya Tatu, haitarajiwi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne italegeza kamba na kupuuza misingi iliyotuletea mafanikio tunayojivunia. Najua mengi yamesemwa na watu wanaodai wanamfahamu Jakaya Mrisho Kikwete na jinsi atakavyolegeza mambo. Napenda kuwahakikishieni kuwa watu hao wamepotea sana.
Wakati wa kampeni wapo baadhi ya wapinzani waliothubutu, kwa kukosa shukrani, kusema ati Serikali ya Awamu ya Tatu ilikuwa inatekeleza sera zinazobuniwa Washington. Serikali ya Awamu ya Nne haitaogopa kubuni na kutekeleza sera na mikakati ya maslahi kwa ukuaji wa uchumi na maisha bora kwa kila Mtanzania ati kwa vile zinaungwa mkono au kufadhiliwa na nchi tajiri na mashirika ya fedha ya kimataifa.
Hatutafanya lolote lisilo na maslahi kwa taifa letu kwa kuwaogopa au kutaka kujipendekeza kwa wakubwa hao. Lakini vile vile hatutaacha kufanya lolote la maslahi kwa taifa na Watanzania kwa vile tu linaenda sambamba na ushauri wa mashirika ya fedha ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika:
Mbali ya kusukumwa na hoja ya kukuza uchumi haraka ili kupiga vita umaskini, tunasukumwa pia na ukweli wa nguvu za utandawazi na ushindani mkubwa katika masoko ya kanda na ya kimataifa. Hivyo basi, sote tuunganishe nguvu zetu ili tuongeze uzalishaji, tuongeze uwekezaji, tuongeze mauzo nje, tuongeze ubora wa mazao na huduma zetu na tuongeze kasi ya ukuaji wa uchumi wetu ili upae.
Michezo, na Burudani na Utamaduni
Mheshimiwa Spika:
Michezo ni furaha. Michezo ni muhimu kwa afya zetu. Watanzania wanapenda sana michezo, ila furaha imekuwa inawakwepa kwa timu zetu kutokufanya vizuri. Lazima tutoke huko na inawezekana. Tutahimiza maendeleo ya michezo shuleni na pale inapowezekana katika sehemu za kazi. Shule ziwe mahali pa kubaini vipaji vya sanaa na michezo na kuiendeleza.
Tutaviwezesha vyama mbalimbali vya michezo ili Tanzania iweze kuwa mshiriki vizuri, na siyo kuwa msindikizaji, katika mashindano mbalimbali ya michezo ulimwenguni. Pamoja na hayo nitaanzisha mjadala wa kitaifa wa kuendeleza michezo nchini. Wadau wote washiriki, na Watanzania, tukubaliane juu ya mstakabali wa michezo nchini mwetu.
Tutaendeleza sekta ya utamaduni na burudani kwa jumla. Miongoni mwa mambo ambayo tutayaangalia kwa karibu ni haki na maslahi ya wasanii ili kazi kubwa waifanyayo iwe na tija kwao.
Mheshimiwa Spika:
Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na duniani.
Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya lugha zake kuu. Aidha Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakua nje ya mipaka ya Afrika.
Mipango Miji
Mheshimiwa Spika:
Kuendeleza miji ni jambo tutakalolipa uzito unaostahili ili tuwe na miji mizuri, safi na salama. Sote tumeona jinsi ambavyo dhana ya mipango miji inavyopuuzwa na kukiukwa na baadhi ya wananchi wetu, manispaa na halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika:
Tusipozuia hali hiyo, miji yetu itakuwa kama pori la majengo yasiyo na mpangilio wala huduma zinazohitajika. Serikali ya Awamu ya Nne itazitaka Halmashauri zote zishughulikie jambo hili haraka inavyowezekana.
Tutaangalia uwezekano wa kuanzisha upya chombo cha fedha kitakachotoa mikopo ya kujenga na kununua nyumba.
Huduma za Kiuchumi
Kuendeleza huduma za kiuchumi za barabara, nishati, simu na kadhalika itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne. Serikali za Awamu zilizotangulia zilisimamia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikijumuisha barabara, vivuko na madaraja. Kwa kuzingatia hoja ya kuunganisha nchi na kuibua maeneo mapya yenye uwezo wa kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kwa kasi upembuzi yakinifu, usanifu, na ujenzi wa barabara na madaraja yote yaliyoorodheshwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005. Tutauimarisha Mfuko wa Barabara ili uendelee kuwa nyenzo muhimu ya kuboresha huduma ya barabara nchini.
Nishati
Mheshimiwa Spika:
Nishati ni sawa na chembe za damu mwilini. Tutapanua wigo na aina ya vyanzo vya umeme na nishati kwa jumla ili kuwa na nishati ya kutosha na yenye gharama nafuu kukidhi mahitaji ya uzalishaji viwandani, utoaji wa huduma za kijamii, na matumizi ya nyumbani. Tutayashughulikia kwa kipaumbele cha juu matatizo ya sasa yahusuyo upatikanaji wa umeme nchini.
Mheshimiwa Spika:
Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa Oktoba 2005 inasema wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itaharakisha mradi wa kupata umeme kutoka makaa ya mawe ya Mchuchuma. Na hivyo ndivyo tutakavyofanya. Aidha, Serikali ya Awamu ya Nne itafufua mipango ya umeme wa Mto Rusumo na Stigler’s Gorge. Vile vile tutaharakisha upatikanaji wa umeme kutoka gesi asilia ya Mnazi Bay.
Mheshimiwa Spika:
Lengo la Serikali ya Awamu ya Nne pia ni kuendeleza kazi ya kufikisha umeme katika miji mikuu ya wilaya isiyo na umeme hivi sasa, kuongeza kasi ya kupeleka umeme vijijini kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini, na kuiunganisha Mikoa ya Kigoma na Ruvuma katika gridi ya Taifa.
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Spika,
Awamu ya Kwanza ya uongozi wa nchi yetu iliweka misingi endelevu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Misingi hiyo ni ujirani mwema, ulinzi wa mipaka yetu, kuwasaidia wakimbizi na kuwa mtetezi wa wanyonge. Awamu zilizofuatia zimefanikiwa kuendeleza misingi hiyo. Serikali ya Awamu ya Nne nayo itaendeleza misingi hiyo pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ambayo inalenga zaidi kwenye diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kwa dhati mazungumzo ya kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki litakalotunufaisha sote sawia. Serikali ya Awamu ya Nne pia itaendeleza ushiriki wetu na uhusiano wetu na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tutahakikisha pia kuwa Tanzania inaendelea kushiriki kwa ukamilifu na kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Afrika, inaendelea kushiriki kwa ukamilifu katika utatuzi wa migogoro Barani Afrika, na hususan katika mchakato wa amani na maendeleo kwenye Kanda ya Maziwa Makuu.
Mheshimiwa Spika:
Tanzania itaendelea kushiriki kwa ukamilifu kwenye shughuli za Umoja wa Mataifa. Hivi sasa nchi yetu ni mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuanzia kesho kutwa, Januari 1, 2006, Tanzania itashika nafasi ya Urais wa Baraza hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja. Katika kipindi hicho Tanzania inatarajia kuleta ajenda ya usalama na usuluhishi wa migogoro katika Eneo la Maziwa Makuu ili lijadiliwe na Baraza hilo. Kadhalika, tutaongeza ushiriki wa Jeshi letu katika Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Ulinzi na Usalama
Mheshimiwa Spika:
Amani na utulivu wa nchi yetu ni moja ya agenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne. Maendeleo ya uchumi pia yanategemea sana utulivu wa nchi. Pamoja na matukio ya hapa na pale nchi yetu kwa jumla imetulia, na ni wajibu wetu kuuendeleza utulivu huu, kwa kufanya yafuatayo:
Kwanza, kujenga mazingira mazuri ya kazi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama;
Pili, kuendeleza juhudi za kuwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama yaliyo imara yenye nidhamu ya hali ya juu na utii, na yenye utaalam na zana za kisasa;
Tatu, kuongeza uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ujambazi na kuzagaa kwa silaha ndogondogo ambazo zinatumika kufanyia uhalifu dhidi ya raia wema. Tatizo hili tutalivalia njuga.
Nne, kuanzisha na kutoa vitambulisho vya uraia; na
Tano, kuongeza kasi ya urejeshaji wa wakimbizi makwao.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge:
Nimesema mengi. Kwa leo inatosha. Ninamalizia kwa kuwahakikishieni kuwa nafahamu vizuri sasa ukubwa wa heshima na uzito wa majukumu niliyokabidhiwa na Watanzania wenzangu. Ninafahamu matarajio ya Chama changu, Chama Cha Mapinduzi. Nitaongoza kwa dhati utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi, na kwa dunia. Ninayajua matarajio ya Watanzania wenzangu walipoitikia wito wa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Ninayajua matarajio ya nchi jirani, bara la Afrika na dunia kwa Awamu ya Nne ya uongozi wa taifa letu. Ninajua wahisani wetu na wawekezaji, wa ndani na nje, wananisikiliza kwa makini, wakitaka kujiridhisha iwapo nitavijaza viatu alivyoniachia Rais wetu mpendwa wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa. Nitajitahidi ingawa ni vikubwa kwangu.
Kwenu nyote, na kwao wote, naahidi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na kwa ushirikiano na Bunge hili na wananchi kwa ujumla, kuwa naweza kutimiza matarajio ya kila mmoja.
Tanzania yenye neema tele inawezekana. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake.
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Post a Comment