0


Mabingwa wa Tanzania bara timu ya Yanga imefanikiwa kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya Kagame Cup baada ya kuifungashia virago KMKM ya Zanzibar kwa kuichapa goli 2-0 kwenye mchezo wa kundi A uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa Yanga dhidi ya K
MKM ulikuwa mgumu na wa vuta nikuvute kwani kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu hizo kufungana, Yanga walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini walishindwa kuzitumia nafasi hizo kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini pindi walipokuwa wakipata nafasi hizo.
Yanga vs KMKMMalimi Busungu aliifungia Yanga goli la kwanza dakika ya 57 kipindi cha pili baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la KMKM ndipo mshambuliaji huyo akaukwamisha mpira kambani. Hilo ni goli la tatu kwa Busungu akiungana na Michael Olunga wa Gor Mahia ya Kenya pamoja na Salah Eldin Osman Bilal wa Khartoum ya Sudani wote wakiwa wameshafunga magoli matatu kila mmoja.
Goli la pili la Yanga lilipachikwa wavuni na Amis Tambwe dakika ya 72 kipindi cha pili aliyeingia kuchukua nafasi ya Malimi Busungu. Wachezaji wengine walioingia walikuwa ni Joseph Zutah aliyeingia kuchukua nafasi ya Juma Abdul na Mbuyu Twite akampisha Andrey Coutinho.
Yanga vs KMKM 6Baada ya mchezo kumalizika Donald Ngoma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa leo (man of the match) baada ya kuonesha kiwango cha juu japo hakufanikiwa kufunga goli. Ikumbukwe kuwa, mchezo uliopita Ngoma alitolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kuoneshwa kadi mbili za njano na alikosa mchezo wa Jumatano Yanga ilipocheza dhidi ya Telecom ya Djibouti.
Matokeo ya leo yanaifanya KMKM iungane na Telecom kuyapa mkono wa kwaheri mashindano hayo kutoka kundi A na kuziacha Khartoum, Gor Mahia na Yanga zisonge mbele kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Yanga vs KMKM 5
Mchezo uliotangulia ulizikutanisha Khartoum dhidi ya Gor Mahia ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1 kwenye mchezo ulipigwa majira ya saa 8:00 mchana.
Kesho michuano hiyo itaendelea tena kwa kuzikutanisha timu za Kundi C ambapo mchezo wa kwanza utakaoanza saa 8:00 mchana utakuwa ni kati ya KCCA ya Uganda dhidi ya Malakia ya Sudan Kusini wakati wawakilishi wengine wa Tanzania timu ya Azam FC itakuwa ikipambana na Adama City ya Ethiopia kuanzia saa 10:00 jioni, michezo yote itapigwa kwenye uwanja wa Taifa.



Post a Comment

 
Top