Mabingwa wa Tanzania bara timu ya
Yanga imefanikiwa kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya
Kagame Cup baada ya kuifungashia virago KMKM ya Zanzibar kwa kuichapa
goli 2-0 kwenye mchezo wa kundi A uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa Yanga dhidi ya K
MKM
ulikuwa mgumu na wa vuta nikuvute kwani kipindi cha kwanza kilimalizika
bila timu hizo kufungana, Yanga walitengeneza nafasi nyingi za kufunga
lakini walishindwa kuzitumia nafasi hizo kutokana na washambuliaji wake
kukosa umakini pindi walipokuwa wakipata nafasi hizo.
Malimi
Busungu aliifungia Yanga goli la kwanza dakika ya 57 kipindi cha pili
baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la KMKM ndipo mshambuliaji
huyo akaukwamisha mpira kambani. Hilo ni goli la tatu kwa Busungu
akiungana na Michael Olunga wa Gor Mahia ya Kenya pamoja na Salah Eldin
Osman Bilal wa Khartoum ya Sudani wote wakiwa wameshafunga magoli matatu
kila mmoja.
Goli la pili la Yanga
lilipachikwa wavuni na Amis Tambwe dakika ya 72 kipindi cha pili
aliyeingia kuchukua nafasi ya Malimi Busungu. Wachezaji wengine
walioingia walikuwa ni Joseph Zutah aliyeingia kuchukua nafasi ya Juma
Abdul na Mbuyu Twite akampisha Andrey Coutinho.
Baada
ya mchezo kumalizika Donald Ngoma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa
mchezo wa leo (man of the match) baada ya kuonesha kiwango cha juu japo
hakufanikiwa kufunga goli. Ikumbukwe kuwa, mchezo uliopita Ngoma
alitolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kuoneshwa kadi mbili za njano
na alikosa mchezo wa Jumatano Yanga ilipocheza dhidi ya Telecom ya
Djibouti.
Matokeo ya leo yanaifanya KMKM
iungane na Telecom kuyapa mkono wa kwaheri mashindano hayo kutoka kundi A
na kuziacha Khartoum, Gor Mahia na Yanga zisonge mbele kwenye hatua ya
robo fainali ya mashindano hayo.
Mchezo uliotangulia
ulizikutanisha Khartoum dhidi ya Gor Mahia ambapo timu hizo zilitoka
sare ya kufungana goli 1-1 kwenye mchezo ulipigwa majira ya saa 8:00
mchana.
Kesho michuano hiyo itaendelea
tena kwa kuzikutanisha timu za Kundi C ambapo mchezo wa kwanza
utakaoanza saa 8:00 mchana utakuwa ni kati ya KCCA ya Uganda dhidi ya
Malakia ya Sudan Kusini wakati wawakilishi wengine wa Tanzania timu ya
Azam FC itakuwa ikipambana na Adama City ya Ethiopia kuanzia saa 10:00
jioni, michezo yote itapigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Post a Comment