0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ameahidi kutoa  kiasi cha sh Millioni moja  kwa kila goli litakalofungwa na Serengeti Boys katika mechi ya marudiano nchini Congo Brazaville.

Ametoa ahadi hiyo wakati akiongea na kuwapongeza wachezaji hao mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Serengeti Boys ya Tanzania na Congo Brazaville uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

“Kwa niaba ya Watanzania wote nawapongeza kwa mchezo mzuri mliouonesha na kuibuka na ushindi lakini bado mnatakiwa kujituma kama mlivyofanya katika mechi hii na naahidi kutekeleza ile ahadi yangu ya laki tano kwa kila goli na nitatoa tena kwenu Millioni moja kwa kila goli mtakalofunga Congo Brazaville.”Alisema Mhe. Waziri Nape.

Kwa upande wa Kocha wa Timu hiyo Bw. Bakari  Shime ameshukuru Waziri na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo na watahakikisha wanapata ushindi katika mechi ya marudiano kwani wameshayaona mapungufu yaliyojitokeza na watayafanyia kazi wachezaji watakuwa tayari kuivaa tena Congo Brazavile.

Aidha Nahodha wa Timu  hiyo Bw. Issa Abdi Makame mbali na kuishukuru Serikali kwa motisha inayotoa ameahidi kujituma zaidi kwa kushirikiana na wenzake na  kufuata maagizo kutoka   Bechi la ufundi  ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa marudiano.

“Tunashukuru sana kwa motisha mnayotupa na sisi hatutawaangusha tutajituma kadri ya uwezo wetu tupate ushindi  tukiwa ugenini ili tuweze kufuzu” Aliongeza Nahodha Makame.

Timu ya Taifa ya Tanzania ya  vijana chini ya  umri wa Miaka kumi na saba (Serengeti Boys) inayowania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana yatakayofanyika nchini Madagascar mwaka 2017 inatakiwa kupata ushindi ili kujihakikishia kufuzu kwa fainali hizo.

Post a Comment

 
Top