0





Serikali imepokea taarifa za kutekwa kwa malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jana tarehe 14 Septemba 2016. Kati ya malori hayo na
ne yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Bw. Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.

Kwa taarifa zilizopatikana watekaji ni kikundi cha waasi cha MaiMai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Bw. Dewji. Waasi hao wametoa saa 24 kuanzia jana saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia.

Wametishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi hicho cha fedha wanachokitaka itakapofika saa 10 jioni leo. Katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania wamefanikiwa kutoroka ambao ndio waliosaidia kutoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshachukua hatua za awali za kuwasiliana na Serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa haraka iwezekanavyo wakiwa salama kabisa.

Tukio hili ni la pili kutokea katika miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2015 Mashekhe kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa Serikali hizi mbili zilifanikisha mashekhe hao kuachiwa huru bila madhara yoyote.

Serikali ingependa kuushauri Umma wa Watanzania hususan wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Congo hususan Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 15 Septemba 2016.

Post a Comment

 
Top